WAZIRI MKUU: MADIWANI WASIPEWE FEDHA ZA MAENDELEO MKONONI
*Asema kama tabia hiyo ilikuwepo, mwisho wake ni jana
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Manispaa nchini kuacha kutoa fedha taslimu na kuwapa madiwani ili zikafanye kazi za maendeleo.
Badala yake amewataka waandae mfumo maalum wa kutoa fedha hizo kama zinavyotolewa fedha za mfuko wa Jimbo ambazo ni maalum kwa wabunge lakini zinatumika kwa shughuli za maendeleo jimboni.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo Manispaa ya Songea.
“Nimepata taarifa kuwa fedha za maendeleo kwa madiwani zinakabidhiwa mkononi. Hapana. Msiwape fedha mkononi, bali zifuate mfumo wa utoaji fedha wa Serikali. Kama mlikuwa na matumizi ya aina hiyo, mwisho wake ni jana,” amesisitiza.
“Fedha za mfuko wa Jimbo ni za Mbunge lakini hapewi mkononi bali zinapelekwa kwenye Halmashauri na yeye anahusika kwenye kikao cha maamuzi. Anakubaliana na madiwani wenzake ni miradi ipi ipatiwe fedha, ambayo mara nyingi inakuwa imekwishaidhinishwa na vikao husika,” ameongeza.
Alisema makusanyo ya fedha yanayofanywa na Halmashauri hayana budi kuangaliwa pia na jinsi fedha hizo zinavyotumiwa. “Lazima tukishakusanya tuangalie tumepata kiasi gani, siyo kukaa na kuamua kutoa sh. laki tano tano kwa kila diwani. Suala la matumizi ni muhimu sana, ni lazima fedha hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo,” amesisitiza.
Amesema kuna baadhi ya watu wanaamua kugawana fedha kwa kigezo cha maendeleo lakini wanaishia kutumia fedha hizo kwa kigezo cha kujengeana uwezo (capacity building). “Hii si sahihi na jana nimepiga marufuku posho za aina hii pamoja na fedha za vitafunwa kwa sababu zinaishia kwa wakubwa wachache na waliozikusanya hawapati chochote,” ameongeza.
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri, Waziri Mkuu amewataka waangalie baadhi ya makampuni ambayo yanajitokeza kutoa vifaa vya kukusanya ushuru lakini wanatumia software ambazo zinawanufaisha na wao pia.
“Tumieni watu wenu wa TEHAMA kukagua mifumo hii kwani kuna baadhi ya watu wanaoleta zile mashine siyo waaminifu. Watu wa TEHAMA wazikague na kujiridhisha kuwa hakuna mianya ya wizi. Tumegundua wako wanaokusanya fedha, lakini asilimia 80 inangia kwenye akaunti za Halmashauri na asilimia 20 inapelekwa sehemu wanayoijua wao. Ukiangalia unaona mapato yanaongezeka lakini kumbe pia unaibiwa. Jaribuni kuchunguza na mjiridhishe na hizo software zao,” amesisitiza.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, JANUARI 4, 2017.
TANGAZO
0 comments:
Post a Comment