Na Mwandishi wetu, Dodoma
Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana
wa CCM) Shaka Hamdu Shaka (MNEC) Septemba 7, 2017 Amezindua Programu
maalumu kwa Vijana wa CCM katika ushiriki wa shughuli za miradi ya
Kimaendeleo, Kiuchumi na Kijamii katika ukumbi wa CCM (NEC) Mjini
Dodoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo
Shaka alisema Wazo hilo limeibuliwa wakati muafaka huku serikali ya CCM
awamu ya tano chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ikiweka mkazo na vipaumbele
kadhaa vinavyomtaka kila mtanzania hususani vijana kujituma, kufanya
kazi kwa bidii na kuzalisha Mali.
Alisema dhana ya kufanya kazi kwa
bidii, malengo na shabaha si ngeni lakini kwa wakati huu inahubiriwa kwa
nguvu kulingana na changamoto nyingi zilizopo, fursa, ushirikishwaji
kwa kuzingatia mahitaji halisi kutokana na mabadiliko ya dunia Kiuchumi
na Kimaendeleo.
Aliwasisitiza Vijana kutambua wajibu
wa kukuza shughuli za kazi na maisha zikiongozwa na nguvu ya uzalendo,
kujali utaifa na kutambua dhamana iliyopo ya kudumisha amani, Umoja,
Mshikamano na Maendeleo.
"Ili kusihi yote hayo hatimaye
Vijana waweze kuyafanikisha tunapaswa kuwa na mioyo isiyopwaya au kukosa
rutuba ya kutodumisha uzalendo, tunalazimika kwa pamoja kutambua mpango
wowote wa kuyafikia maendeleo ya kweli utabaki ni hadithi na ndoto Kama
hatutaongozwa na shime ya uzalendo au kutothamini utaifa wetu Kama
ambavyo viongozi wanatuhimiza siku Hadi siku" Alisema Shaka
Shaka aliwaeleza Vijana kuwa pamoja
na kuwepo juhudi kubwa za mara kwa mara kuchukuliwa na serikali,
mashirika hiari ya Kijamii na yasiyokuwa ya kiserikali, kuelimisha juu
ya dhana ya ushirikishwaji na ushiriki wa Vijana katika miradi ya
Kiuchumi na Kijamii wanapaswa kuwa na utayari, uthubutu, uzalendo, na
Utaifa.
Alisema kuwa Vijana wanapaswa
kukubali kujadiliana na wenzao juu ya mpango wa maendeleo na hatma ya
Taifa na mustakabali wake kwani ndiyo njia pekee ya kukuza uzalendo kwa
Taifa.
Alisema mataifa yaliyoendelea
yametokana na watu wake kukubali kufanya kazi kwani Ndiko kuliko
yakomboa mataifa hayo yaliyoendelea kutoka katika uchumi duni na kuhamia
katika uchumi wa Kati na Sasa wakionekana kuwa na uchumi wa maendeleo
ya viwanda.
"Mafanikio hayakuja Kama zawadi
kwenye kisahani Cha Chai ama kutokea kwa bahati mbaya Kama mtende
unavyoota jangwani ni lazima kukubali kwa pamoja kufanya kazi ili
kupambana na adui umasikini"
"Wakati huu ambao serikali imebeba
mzigo wa kutoa elimu bure toka msingi Hadi sekondari ni lazima Vijana
tuwe na muktadha mmoja wa kujenga mtazamo wa pamoja kwa kujitambua na
kukubali kufanya kazi bila kusukumwa" Alisema Shaka
Aliongeza kuwa kazi ya Vijana siku
zote na kila wakati inapaswa kuwa ni kufikiri, kupambanua, kubuni na
kujadiliana ili kumaliza changamoto, vikwazo, fursa na matumizi ya
nafasi husika katika Jamii.
Aidha, kupitia kusanyiko hilo
aliwaagiza na kuwataka makatibu wote wa Umoja wa Vijana wa CCM wa mikoa
na Wilaya nchini kila mmoja kuhakikisha programu hiyo inaanzishwa katika
mikoa na Wilaya zake na kusisitiza kuhitajika matokeo makubwa kwani
ataandaa utaratibu wa kuthamini programu hiyo kila kipindi Cha robo
mwaka.
Sambamba na hayo pia Kaimu Katibu
Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Ndg Shaka Hamdu Shaka
alishiriki ujenzi wa shule ya Msingi Mizengo Pinda iliyopo katika Kijiji
Cha Chinangali 2 Kata ya Bwigili Wilayani Chamwino.
Pamoja na kushiriki shughuli ya
uchimbaji msingi, ufyatuaji tofali na matengenezo ya tungilizi kwa ajili
ya upauaji wa majengo ya shule hiyo pia Shaka alichangia mifiko 20 ya
saruji kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi walizozianza kwa
kujitolea nguvu, muda na rasilimali zao.
|
Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM) Shaka Hamdu Shaka (MNEC) akizndua programu hiyo. |