SERIKALI YAANZA MCHAKATO WA UJENZI WA RELI YA KATI KWA KIWANGO CHA KIMATAIFA (STANDARD GAUGE)
Na Frank Shija, MAELEZO.
Serikali ya Awamu ya Tano ndani ya mwaka mmoja imeanza mipango ya kuboresha usafiri wa reli ya Kati kwa kuijenga kwa kiwango cha kimataifa yaani Standard Gauge. Usafiri huu utaongeza fursa za kiuchumi kwani mazao ya chakula na biashara toka mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Singida kuelekea Dar es Salaam yatasafirishwa kwa haraka.
Reli hii itarahisisha pia usafiri wa abiria wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kati na Magharibi. Usafiri wa treni kwa kiwango kikubwa huwa ni wa uhakika na wa gharama nafuu. Hivyo ujenzi wa reli kwa Standard Gauge uteleta ukombozi mkubwa wa kiuchumi kwa watu wa maeneo hayo na Taifa kwa ujumla.
Kwa kipindi kirefu huduma ya usafiri wa treni kupitia Reli ya Kati (Central Line Railway) imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma na maeneo ya Kanda ya ziwa na nchi za jirani zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Historia inaonesha kuwa Reli ya Kati kama inavyojulikana sasa ilijengwa kati ya mwaka 1905 hadi 1914 wakati huo ikiitwa Reli ya Tanganyika kwa kuwa ilikuwa ikielekea Mkoani Kigoma ambako Ziwa Tanganyika linapatikana.
Kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi kupitia usafirishaji bidhaa na huduma mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imeamua kuja na mpango kabambe wa kuifanyia maboresho miundombinu ya reli hiyo ili iweze kwenda na wakati na kasi ya ukuaji wa uchumi.Mpango huo unahusisha ujenzi wa mtandao wa Reli mpya ya Kati katika Viwango vya Kimataifa (Standard Gauge 80’) ili kuendana na kasi ya ongezeko la mizigo.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bw. William Budoya anaeleza kuwa gharama iliyokaidiriwa kutumika kukamilisha mradi huo ni Dola za Kimarekani Bilioni 7.6 ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 16.Fedha hizo zitatumika kugharamia ujenzi wa Kilomita 2,561 za reli kwa kiwango cha Kimataifa . Ili kufanikisha mradi huo Serikali imepata ufadhili kutoka Benki ya Exim ya China ambayo imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa ujenzi huo unafanikiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao Rais wa benki hiyo anamuhakikishia Rais Dkt. John Magufuli kuwa Benki hiyo iko tayari kutoa kiasi hicho cha fedha ili kufanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli. Pia anamuhakikishia Rais kuwa Benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli hiyo.Akiuzungumzia ujenzi wa Reli hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anabainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Anasema reli hiyo mpya itakua tofauti na inayotumika sasa kutokana na uwezo wake wa kuhimili usafirishaji wa mizigo mingi kwa kuwa inajengwa kwa kiwango cha Kimataifa "Standard Gauge railway " na itaanzia Dar es Salaam Mpaka Kigoma, kupitia Tabora, Mwanza,Isaka hadi Rusumo; Kaliua -Mpanda -Karema na Uvinza -Musongati nchini Burundi.
Katika ufafanuzi alioutoa hivi karibuni kuhusu ujenzi wa reli hiyo wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi mjini Dodoma hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli alisema tayari mchakato wa ujenzi wa reli hiyo umeanza kwa kutangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakaye jenga Reli hiyo.
Anasema sambamba na kazi hiyo Serikali itakarabati matawi ya reli ya kati sehemu ya Kaliua-Mpanda ili kuboresha ufanisi wake, kwa kutenga Sh. bilioni 5.5 za ajili ya usanifu.Aidha, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano uliowasilishwa bungeni Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango unaeleza kuwa Serikali imejipanga kufanya usanifu na ujenzi wa madaraja 16 kati ya 28 yaliyochakaa kati ya Dar es Salaam na Tabora.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servaciaus Likwelile akizungumza mara baada ya utiaji saini wa makubaliano wa ujenzi wa reli hiyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Naibu Meneja Mikopo Nafuu wa Benki ya Exim ya China Bw. Zhu Ying anasema kuwa Dola za Kimarekani bilioni 7.6 ambazo ni sawa na Shilingi Trilioni 16 zitatumika kutekeleza mradi huo.
Dkt. Likwelile anasema hatua hiyo inawezesha kuanza kwa kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu na uundwaji wa timu za pamoja kuanza kuainisha mahitaji halisi ya ujenzi wa mradi huo.Anasema mradi huu umekuja wakati muafaka kutokana na kwamba reli iliyopo sasa ambayo ni ya Kiwango cha "meter gauge” haina uwezo mkubwa katika ubebaji wake wa mizigo, hata baada ya kufanyiwa ukarabati.Kwa mwaka ni tani Milioni 5 za mizigo ndizo zinaweza kupitishwa na reli ya sasa, ambazo haziwezi kukabili mahitaji ya mizigo ya Kanda hii ambayo itafikia tani Milioni 30 ifikapo mwaka 2025.
Kutokana na uhitaji huo wa kukabiliana na uongezaji wa mizigo kwa kujenga uwezo wa kuihudumia kwa kuwa na reli ambayo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba mizigo hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi na kwa starehe lakini pia kwa kasi ya spidi ya wastani wa kilometa 100 kwa saa hivyo kuwezesha abiria kufika haraka zaidi sehemu wanazokwenda.
Pia wakati wa ujenzi wa reli hiyo watanzania takribani 300,000 watapata ajira kutokana na kushiriki katika ujenzi wa reli hiyo.
TANGAZO
0 comments:
Post a Comment