WAZIRI MUHONGO AKEMEA WIZI WA MALI ZA UMMA, AMWAGA MISAADA YA VIFAA VYA MATIBABU MUSOMA VIJIJINI
Matroni wa Kituo cha Afya cha Murangi, Sabina Daudi akitoa shukrani kwa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) baada ya kupokea vifaa kwa ajili ya kituo hicho.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Thadeus Makwanda na katikati ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Murangi, Dkt. Josephat Karambo.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiwasili katika Kituo cha Afya cha Murangi kwa ajili ya kukabidhi vifaa mbalimbali. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Vicent Naane.
Baadhi ya Vitanda ikiwa ni miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa katika Kituo cha Afya cha Murangi.
Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesikitishwa na wizi wa dawa na uharibifu wa baadhi ya vifaa katika Kituo cha Afya cha Murangi, Musoma Vijijini na kuagiza wahusika wachukuliwe hatua.
Agizo hilo alilitoa hivi karibuni wakati akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya afya ikiwemo vitanda maalum 10, baisikeli za wagonjwa na vifaa vingine kutoka kwa wafadhili wa Australia kwa ajili ya Kituo hicho na kushuhudiwa na wananchi mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya jimbo hilo.
Awali kabla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, alipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusiana na wizi wa dawa uliomhusisha mlinzi wa Kituo hicho pamoja na tukio la kuharibiwa kwa gari la wagonjwa alilokabidhi mwezi Machi mwaka huu.
Taarifa husika ilimkasirisha Profesa Muhongo na hivyo kuagiza wahusika wote wachukuliwe hatua za kisheria haraka iwezekanavyo ili iwe fundisho kwa wenye tabia za namna hiyo.Akizungumzia gari hilo, Profesa Muhongo alisema lilitolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini lengo likiwa ni kusaidia wananchi hao kuondokana na usumbufu waliokuwa wakiupata.
Aliongeza kuwa Serikali hiyo ya Japan ilimuahidi magari mengine zaidi ikiwa gari hilo litatunzwa vizuri na kutumika kwa shughuli iliyokusudiwa.“Hii ni aibu kubwa, hata wafadhili watatushangaa na kutucheka, dawa nyingi tulipewa na wafadhili na gari ile tulikabidhiwa ikiwa bado mpya na kwa Tanzania gari za namna hiyo zipo mbili tu, ni hapa na Muhimbili,” alisema.
Mbali na hilo aliongeza kuwa Serikali ya Japan ilitoa kiasi cha shilingi milioni 170 kwa ajili ya kuboresha Kituo hicho na kuongeza kuwa atamuomba Balozi wa Japan nchini kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hiyo.Aliwaagiza Madiwani kufuatilia kubaini hatua iliyofikiwa ya matumizi ya fedha hiyo na alisema endapo itadhihirika kuna ubadhirifu wa aina yoyote hatua za kisheria zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kurejesha fedha hizo.
Profesa Muhongo alisema anashangazwa kupewa taarifa hiyo na wananchi huku viongozi wakiwa kimya bila kuonesha hatua walizochukua na hivyo aliwataka Madiwani kutokuwa waoga katika kuwachukulia hatua wanaofanya ubadhirifu.Aidha, Profesa Muhongo aliwaagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Thadeus Makwanda na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Murangi, Dkt. Josephat Karambo kuhakikisha hadi kufikia Tarehe 15 mwezi ujao gari hilo liwe limetengemaa.
TANGAZO
0 comments:
Post a Comment