RAIS DKT. MAGUFULI APOKEA TAARIFA YA ZOEZI LA UHAKIKI WA VYETI KWA WATUMISHI WA UMMA MJINI DODOMA
Na Nuru Juma na Beatrice Lyimo-MAELEZO .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watumishi 9932 waliogushi vyeti, kuondoka maeneo yao ya kazi haraka iwezekanavyo kabla hawajadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akikabidhiwa taarifa ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma sambamba na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka kumi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Watumishi 9932 wenye vyeti vya kugushi na feki mishahara yao ya mwezi huu ikatwe na waondoke kazini mara moja na hizo nafasi zitangwazwe ili wasomi waweze kuziomba na majina yao yawekwe kwenye magazeti ili wajulikane” amesema Rais Magufuli
Aidha amesema kuwa hadi kufika tarehe 15 Mei, 2017 kila mkuu wa Idara mahali pake pa kazi ahakikishe watumishi hao wameondoka na watakao kaidi agizo hilo amevitaka vyombo vya usalama kuwashughulikia.
Hata hivyo Rais Magufuli ameongeza kuwa watumisi 1538 wanaotumia cheti zaidi ya mtu mmoja kutopewa mshahara hadi pale itakapojulikana nani mwenye cheti halali na kuwataka watumishi 11,769 kuwasilisha vyeti vilivyopungua.
Mbali na hayo Rais Magufuli amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kuachana na masuala ya siasa kwa lengo la kujenga nchi kwani watanzania wanahitaji maendeleo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Angela Kairuki amesema kuwa mpaka sasa vyeti vilivyohakikiwa ni 435,000 ambapo imefanyika kwa awamu tatu iliyojumuisha Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma, Tume na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi na Wakala wa Serikali pamoja na Serikali Kuu.
“Leo tunakabidhi taarifa ya awamu mbili iliyohusisha Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma, Tume na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi na Wakala wa Serikali ambapo imejumuisha uhakiki wa vyeti vya Kidato cha Nne, Sita, vyeti vya ualimu kwa ngazi ya cheti na stashahada” amesema Waziri Kairuki.
Amesema kuwa matokeo ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma yapo ya aina nne ambapo watumishi 376,969 sawa na asilimia 94.23 wanavyeti halali, watumishi 9932 asilimia 2.4 wanavyeti vya kugushi, watumishi 1538 asilimia 0.3 vyeti vyao vinatumika kwa zaidi ya mtu mmoja na watumishi 11,769 asilimia 2.8 wanavyeti pungufu.
Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alisema wizara yake inakumbana na changamoto ya watumishi wa umma kugushi vyeti hivyo aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwani serikali imeziba njia zote za mkato za kuajiriwa na Serikali.
“Leo tunaandika historia ya kipekee kwani suala la uhakiki wa yveti limefanyika kwa mara ya kwanza nchini ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndio yenye jukumu la kuhakiki uhalali wa vyeti hivyo” amesema Prof. Ndalichako.
Zoezi la uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma limeendeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia Mwezi Oktoba, 2016 likiwa na lengo la kubaini uhalali wa vyeti kwa watumishi wake.
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akinyanyua juu Taarifa na
vitabu vye majina 9,932 ya watumishi wenye vyeti vya kugushi.
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe na kufungua
boksi kubwa lenye majina ya watumishi zaidi ya 9,932 waliobainika kuwa na vyeti
vya kugushi mara baada ya kupokea Taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma kutoka kwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela
Kairuki katika Ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa , Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako, Spika
wa Bunge Job Ndugai, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala bora Angela Kairuki wakiminya kitufe kuashiria maadhimisho ya
miaka 10 ya Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan akihutubia katika Ukumbi wa Chimwaga.
|
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akihutubia katika hadhara hiyo katika Chuo kikuu cha Dodoma
UDOM.
Baadhi ya
viongozi mbalimbali wakifatilia kwa makini Hotuba iliyokuwa ikitolewa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika maadhimisho
ya miaka 10 ya Chuo cha UDOM toka kuanzishwa kwake.
Baadhi ya
Makatibu wakuu pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanafunzi pamoja na
walimu wa UDOM wakipiga makofi wakati
wakimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
wakati akiwasili katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya miaka 10 ya Chuo kikuu cha Dodoma UDOM kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula, katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma. (PICHA NA IKULU)
TANGAZO
0 comments:
Post a Comment